Friday, September 24, 2010

ULIVYOKUWA MGOMO ULE


(Mgomo wa Chuo Kikuu Moi, 2009)
Mlipuko. Rabsha. Watu kukimbizana, kukanyagana. Majibwa. Jekejeke. Kulikoni? Hapakuwa na wakumjibu mwengine. Kila mmoja akaiswafia nia kauli ya mguu niponye. Naam, mguu uliponya wengine; ila wengine waso kismati waliyaona machungu uso kwa macho. Polisi, polisi, polisi. Kama waliotumwa na malaika Izraili, walitaka kulipasua fuvu lolote walilolipata. Kukawa ni tandabelua isiyoelezeka kwa maneno. Kweli, baada ya kisa mkasa.

Seng’enge zikawa pingamizi kubwa. Mwenzangu, unapofukuzwa na askari aliyebeba kigongo kilicho ngangari kuliko cha mvule, inabidi ujinusuru. Wasemao husema mbwa hafi maji akiona ufuko. Basi iweje: ufuko upo, ila seng’enge zimeukinga. Nazo hazitaki kubanduka ng’o! Ni hali ya kutamausha. Majibwa ya polisi nayo yalikuwa na ari ya kumng’ata yeyote bila simile. Kukanyagana ndiko huko. Kusahauliana. Kutweta. Kutokwa na jasho. Kifo. Naam, kifo.

Wengine wakaamua kuingia kwenye shamba la ngano. Kujinusuru eti. Laiti wangelijua. Askari waliwafuata kenyekenye na wengi wao walipata kulionja rungu lile. Ni rungu ambalo dhoruba lake li chungu kuliko mikuki yote ya nguruwe duniani. Hata mmoja kaonekana kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti la Nation. Akipokea gongo. Mabinti walizirai; si mmoja si wawili—mabinti lukuki. Na wengi walipokea marungu pasi huruma. Vilio. Yupo mmoja aliyezimia, akaamka usiku wa manane; akajipata asikokujua. Mtume! Pengine wapo waliobakwa. Pengine.

Wengine haooo, kwenye mashamba ya mahindi. Na mashamba ya janibu hizi si vishambavishama; ni mashamba maddal-basari. Vitoamachozi viliwaandama huku wakienda matiti. Dafrau! majibwa yaliwabwaga chini wengine, na bila shaka walioshikwa kwa njia hiyo walikiona kilichomfanya sangara kuchomwa moto. Na usidhani waliotoroka walikuwa wakijua waendako. Ilibidi kuzihepa tariki kwani askari walikuwa wakipita kule na magari yao, marungu mikononi. Basi, wengi wakatorokea wasikokujua wala kukufahamu. Na ilikuwa mbali na chuo. Mbali. Hebu tafakari: mtu yuakimbia kuelekea asikokujua, akiruka seng’enge, akikumbana na mifugo, akiruka mashimo. Ilikuwa ni hali ambayo mtu lazima kibuhuti kimpande. Wanakijiji wakawa ndio waauni.

Kutembea walikotembea wanafunzi mosi hiyo hakuwezi kumithilishwa na chochote. Ikawabidi wengi kupita mbali; hadi Kesses Dam. Wakakifuata kijito kitokacho huko hadi kuitwako Falls. Ndipo wakafuata vichochoro wakarudi chuoni, hoi bin tiki punda wa dobi kando. Yakhe, angurumapo simba, mcheza ni nani?

Ndipo katika msukosuko ule, kundi moja likaona upenyu. Upi? Gari lililokuweko barabarani kule. Halambe-halumbe, wakamtoa dereva ndani kwa nguvu. Mwanafunzi mmoja akaushika usukani. Wengine wakaliabiri gari. Kwa fujo. Wakakaa kotekote, motemote, potepote. Gari likazidiwa ila halikulalama. Lilisalimu amri kwa muda. Likaendeshwa mbiooo, kuelekea hapa chuoni. Faya kun faya, polisi wakatia nari gari lao pia. Wakaanza kuwafukuza wale walioliabiri gari. Kasi. Ndipo maji yalipolizidia unga gari lile na bingiri! likabingiria. Yaliyofuata mauko. Nadhani mwayamaizi fika.


No comments:

Post a Comment